Afisa mmoja wa ngazi za juu wa kijeshi wa Sudan atembelea Ethiopia
(last modified Sat, 22 Jan 2022 14:02:21 GMT )
Jan 22, 2022 14:02 UTC
  • Afisa mmoja wa ngazi za juu wa kijeshi wa Sudan atembelea Ethiopia

Afisa mmoja wa ngazi a juu wa Sudan ametembelea nchi jirani ya Ethiopia wakati huu ambapo nchi hizo mbili zina mzozo mkubwa wa mpaka.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Mohammed Hamdan Dagalo, Naibu wa Mkuu wa Baraza Kuu la Kijeshi la Sudan, amewasili mjini Addis Ababa leo Jumamosi kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Miezi miwili iliyopita, Khartoum ilitangaza kuwa, askari wake wa mpakani wapatao sita walitoweka na mpaka hivi sasa hawajulikani walipo. Sudan inalilaumu jeshi la Ethiopia na wanamgambo wake kuwa ndio waliosababisha kutoweka askari sita wa mpakani wa Sudan. Hata hivyo serikali ya Ethiopia imekanusha madai hayo.

Sudan ina mzozo wa muda sasa wa mpakani na nchi jirani Ethiopia wakati nchi hizo mbili hivi sasa zikiwa zimezongwa pia na migogoro ya ndani.

 

Ukitoa mzozo mkubwa na mapigano ya ndani hasa katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia, kwa huko Sudan wananchi wa nchi hiyio jana Ijumaa waliendelea kufanya maandamano wakipinga majenerali wa jeshi kuendelea kung;ang'ania madarakani ya nchi hiyo na kutoa wito wa kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Maandamano hayo makubwa ya jana yaliyopewa jina la "Ijumaa ya Shahidi" yalifanyika katika mji wa Khartoum na miji mingine muhimu ya nchi hiyo ambayo imekuwa ikishuhudiwa maandamano karibu kila siku.

Wananchi wa Sudan waliandamana hiyo jana baada ya Swala ya Ijumaa wakiitikia wito wa Jumuiya ya Wafanyakazi na asasi nyingine za kiraia kwa ajili ya kuwashinikiza wanajeshi wa nchi hiyo waachie ngazi na kuruhusu demokrasia ichukue mkondo wake.

Tags