Watu 16 wamepoteza maisha Cameroon katika mkasa wa moto
Serikali ya Cameroon imetangaza habari ya kuaga dunia watu wasiopungua 16 katika mkasa wa moto uliozuka ndani ya klabu ya starehe katika mji mkuu wa nchi hiyo, Yaounde.
Taarifa iliyotolewa jana Jumapili na Wizara ya Habari ya nchi hiyo imesema, kwa akali watu 16 wameaga dunia kwenye mkasa huo wa Jumamosi usiku, huku wengine wanane wakipata majeraha mabaya ya kuungua.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, moto huo ulitokana na miripuko ya fataki ndani ya klabu hiyo katika wilaya ya Bastos, ambayo ina majumba na ofisi za kibalozi, viungani mwa mji mkuu Yaoude,

Mashuhuda wanasema baadhi ya wahanga wa mkasa huo waliaga dunia kwa kuvuta moshi mzito uliowasakama, na wengine kutokana na mkanyangano ulioanza baada ya kila moja kukimbia huku na kule kuokoa maisha baada ya moto huo kuanza.
Haya yameripotiwa katika hali ambayo, Cameroon ni mwenye wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), iliyoanza Januari 9 mwaka huu 2022.