Dr. Tulia Ackson achaguliwa kuwa spika mpya wa Bunge la Tanzania
- 
					
									Dr. Tulia Ackson  
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemchagua Dk Tulia Ackson kuwa spika wa bunge hilo.
Dr. Tulia amefanikiwa kuwabwaga wagombea wenzake nane wanaotoka vyama vingine vya kisiasa
Tulia ameshinda kwa asilimia 100 akijizolea kura zote 376.
Tulia aliwahi kuwa Naibu Spika chini ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ambae alijiuzulu mapema mwezi huu wa Januari baada ya kutokea mkwaruzano kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan wa nchi hiyo.
Dr. Tulia anakuwa Spika wa pili mwanamke kuliongoza Bunge la Tanzania.
Alizaliwa katika Kijiji cha Bulyaga, wilayani Tukuyu mkoani Mbeya mnamo Novemba 23 mwaka 1976. Ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika sheria kutoka katika Chuo Kikuu mashuhuri cha Cape Town, Afrika Kusini.
Uchaguzi wa Spika mpya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unafuatia hatua ya spika wa zamani, Job Ndugai, kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kutokea mvutano mkubwa wa kisiasa kutokana na kauli yake aliyoitoa kuhusu hatua ya Rais Samia Suluhu kukopa shilingi trilioni 1.3.
Job Ndugai alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akielezea kuwa Tanzania itapigwa mnada kutokana na mikopo mikubwa inayoendelea kuchukuliwa na serikali.