Feb 05, 2022 04:42 UTC
  • Kimbunga Batsirai kusababisha watu 150,000 kupoteza makazi Madagascar

Huenda watu 150,000 wakakosa pahala pa kuishi kutokana athari za Kimbunga cha Batsirai kinachotazamiwa kukipiga kisiwa cha Madagascar leo Jumamosi.

Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) limesema kimbunga hicho kinachokwenda kwa kasi ya kilomita 200 kwa saa kinatazamiwa kusababisha upepo mkali na mvua kubwa katika maeneo ya pwani ya nchi hiyo.

Jens Laerke, afisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA) ametahadharisha kuwa, kimbunga hicho kinatazamiwa kuitumbukiza Madagascar katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Naye afisa mmoja wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Pasqualina Disirio, amesema shule nyingine zimefungwa katika maeneo ya pwani ya Madagascar, huku wakazi wa maeneo hayo wakigubikwa na hofu kutokana na kimbunga hicho.

Athari za kimbunga Madagascar

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya kimbunga kingine cha kitropiki kwa jina la Ana kusababisha vifo vya watu 58 huku wengine zaidi ya 130,000 wakipoteza makazi yao kisiwani Madagascar.

Madagascar imekuwa ikikumbwa na vimbunga mara kwa mara ambavyo mbali na kusababisha maafa na kupelekea malaki ya watu kuachwa bila makazi, lakini huathiri pia miundomsingi na mifumo ya mawasiliano.

Tags