Amir- Abdollahian: Hakuna ubunifu wowote wa jadi na mkubwa uliowasilishwa na Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa hakuna ubunifu wowote wa jadi na mkubwa uliowasilishwa na Marekani kwa ajili ya kuondoa vikwazo na kurejea katika mapatano ya JCPOA.
Kuhusu taarifa za karibuni kuhusiana na mazungumzo ya kuondoa vikwazo huko Vienna, Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Vitendo vya upande wa pili ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na Marekani inapasa kudhidhirisha wazi na kikamilifu hatua zake za kivitendo za kuondoa vikwazo.
Aidha kuhusu madai ya Robert Malley Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran kwamba Washington imeiainishia Tehran vikwazo ili kuhuisha mapatano ya JCPOA, Amir Adbollahian amebainisha kuwa Iran haijapokea masharti yoyote kutoka upande wa Marekani; na kimsingi kadhia iliyopo si masharti bali mazungumzo yanaendelea kulingana na maoni ya wataalamu na mapatano ambayo natija yake ni kufikia katika makubaliano mazuri na kudhamini maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wakati huo huo amefafanua kuhusu taarifa inayosema kuwa Rais Joe Biden wa Marekani amesaini misamaha kadhaa ya vikwazo kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya kiraia kwa kusema" kile kilicho muhimu kwa Iran ni matokeo ya mazungumzo yanayoendelea huko Vienna na pia makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo hayo.
Duru mpya ya mazungumzo ya Vienna iliyoanza tangu Januari 28 hivi sasa imeakhirishwa ili jumbe ziendelee na mashauriano katika miji mikuu ya nchi zao ili kuchukua maamuzi ya kisiasa yatakayopelekea kufikiwa mapatano.