UN: Ukame umeathiri watu milioni 4.3 nchini Somalia
Umoja wa Mataifa umesema Somalia inaendelea kuandamwa na ukame ambao umeathiri watu zaidi ya milioni 4.3 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, kutoka watu milioni 3.2 iliyoripotiwa mwezi mmoja uliopita.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema, hali ya ukame nchini Somalia imewalazimisha watu 271,000 kuhama makwao.
OCHA imesema hali ya ukame inayozidi kuwa mbaya nchini Somalia imesababisha mamilioni ya Wasomali kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji.
Ofisi hiyo ya UN imeongeza kuwa, kuna hatari kubwa ya kutokea miripuko ya magonjwa kama vile kipindupindu kutokana na uhaba wa maji, huku surua ikisemekana kuongezeka miongoni mwa watu walioko kwenye kambi za wakimbizi.

Hivi karibuni pia, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) ulisema ukame uliolikumba eneo la Pembe ya Afrika unatishia usalama wa chakula wa mamilioni ya watu katika ukanda huo.
Shirika hilo la kuhudumia watoto la UN lilisema watu milioni 6 nchini Ethiopia, na wengine milioni 7 katika nchi jirani ya Somalia wanahitaji misaada ya dharura baina ya sasa na katikati ya mwezi ujao wa Machi.