Serikali ya Kongo na wapinzani wasisitiza kuendelea na mazungumzo ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8017-serikali_ya_kongo_na_wapinzani_wasisitiza_kuendelea_na_mazungumzo_ya_amani
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapinzani wa harakati ya zamani ya waasi ya Machi 23 wamesisitiza kuendeleza mazungumzo ya kusaka amani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2016 02:19 UTC
  • Serikali ya Kongo na wapinzani wasisitiza kuendelea na mazungumzo ya amani

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapinzani wa harakati ya zamani ya waasi ya Machi 23 wamesisitiza kuendeleza mazungumzo ya kusaka amani nchini humo.

Aidha pande hizo mbili zimechunguza makubaliano yaliyosainiwa mjini Nairobi Kenya mwezi Disemba mwaka 2013 kwa shabaha ya kuhitimisha vita nchini humo. Wawakilishi wa pande mbili hizo walikutana katika kikao maalumu mjini Kinshasa.

Hicho ni kikao cha kwanza kufanyika mjini Kinshasa kati ya serikali ya Kongo na harakati ya zamani ya waasi ya Machi 23 kwa kuhudhuriwa na Said Djinit, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu la Afrika, wawakilishi wa Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko Kongo.

Makubaliano ya Nairobi yanajumuisha vipengee kumi kuhusiana na mapatano kati ya serikali ya serikali ya Kongo na harakati ya Machi 23 kuhusu mchakato wa mazungumzo ya kusaka amani. Mchakato huo unajumuisha pia suala la kuanza mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kinshasa na harakati ya Machi 23, upokonyaji silaha na kuwarejesha nchini Kongo kutoka Uganda wanachama wa zamani wa harakati hiyo ya waasi ambao ni zaidi ya elfu mbili.