Nigeria yasajili vifo 59 vya homa ya Lassa tokea Januari 3
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80476-nigeria_yasajili_vifo_59_vya_homa_ya_lassa_tokea_januari_3
Watu wasiopungua 59 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa homa ya Lassa katika sehemu mbalimbali za Nigeria tokea Januari 3 mwaka huu hadi sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2022 23:38 UTC
  • Nigeria yasajili vifo 59 vya homa ya Lassa tokea Januari 3

Watu wasiopungua 59 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa homa ya Lassa katika sehemu mbalimbali za Nigeria tokea Januari 3 mwaka huu hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza cha nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika (NCDC) inasema kuwa, mbali na kufariki dunia watu hao 59 tangu mwanzoni mwa mwaka huu, idadi ya kesi za homa ya Lassa zilizosajiliwa nchini humo hadi sasa ni 358.

Taarifa ya NCDC imeeleza kuwa, watu 19 waliaga dunia wiki iliyopita pekee nchini humo, kwa maradhi hayo yanayoshabihiana sana na ugonjwa wa Ebola na Marbug.

 Watu 102 walipoteza maisha nchini humo kutokana na mripuko mwingine wa homa ya Lassa mwaka jana 2021, ambapo kesi zilizonakiliwa katika mripuko huo ni  674. 

Dalili za homa ya Lassa kuanzia machovu mwilini hadi kuharisha

Homa ya Lassa huenea kwa wanadamu kupitia chakula na vifaa vya ndani ya nyumba vilivyochafuliwa na kinyesi pamoja na mikojo ya wadudu kama panya n.k.

Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1969 katika mji wa Lassa na ndio maana ulipewa jina la mji huo ulioko katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.