28 wajeruhiwa katika maandamano ya Wasudan ya kupinga utawala wa kijeshi
Watu wasiopungua 28 wamejeruhiwa katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imesema leo Ijumaa kuwa, waandamanaji wawili wamejeruhiwa kwa risasi huku wengine sita wakipata majeraha mabaya kwa kugongwa na makopo ya mabomu ya kutoa machozi.
Maelfu ya wananchi wa Sudan jana Alkhamisi waliandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa nchini humo kushinikiza utawala kamili wa kiraia.
Waandamanaji hao walitoa mwito wa kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa haswa waliokamatwa katika maandamano, sanjari na kuwajibishwa waliohusika na mauaji ya waandamanaji.
Takwimu za madaktari zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu karibu 90 wameuawa na mamia ya wengine wameshajeruhiwa katika maandamano hayo ambayo yalianza Oktoba 25 mwaka jana, wakati jeshi lilipotangaza kutwaa madaraka kikamilifu nchini humo.
Maandamano hayo yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi mengine mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021 ambayo yaliiondoa madarakani serikali iliyokuwa inashirikisha pia raia nchini humo.