Chama kilichoondolewa madarakani Burkina Faso chataka Kabore aachiwe huru
Chama cha Rais aliyepinduliwa nchini Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore, kimekita kikosi cha wafanya mapinduzi kilichotwaa madaraka kimwachie huru bila ya masharti yoyote rais huyo wa zamani wa Burkina Faso ambaye yuko katika kifungo cha nyumbani.
Chama hicho kilichoondolewa madarakani nchini Burkina Faso kimetoa wito huo ikiwa umepita mwezi mmoja tangu Christian Kabore atiwe nguvuni na wanajeshi Januari 24 mwaka huu katika mji mkuu Ouagadougou.
Mwenyekiti wa chama hicho Allasane bala Sakande amesema kuwa Chama cha Maendeleo ya Wananchi kina wasiwasi na kinahoji sababu za kuendelea kushikiliwa nyumbani Christian Kabore. Chama hicho pia kimemtaka mkuu wa kikosi cha wanajeshi waliofanya mapinduzi, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, kutekeleza ahadi alizotoa kwamba atahakikisha haki za msingi za kila raia zinalindwa.
Kabore alikamatwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani katika wilaya ya Ouaga 2000 baada tu ya mapinduzi ya jeshi la Burkina Faso.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) zimetoa wito wa kuachiwa huru rais huyo wa zamani wa Burkina Faso.