Wasudan waandamana tena kupinga utawala wa kijeshi, 50 wajeruhiwa
(last modified Fri, 04 Mar 2022 12:17:16 GMT )
Mar 04, 2022 12:17 UTC
  • Wasudan waandamana tena kupinga utawala wa kijeshi, 50 wajeruhiwa

Zaidi ya watu 50 wamejeruhiwa katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo.

Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imesema leo Ijumaa kuwa, waandamanaji 55 wamejeruhiwa kwa risasi huku wengine wakipata majeraha mabaya kwa kugongwa na makopo ya mabomu ya kutoa machozi huko Khartoum na miji ya Gadarif na Dongola. 

Maelfu ya wananchi wa Sudan jana Alkhamisi waliandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa nchini humo kushinikiza kurejeshwa utawala kamili wa kiraia.

Waandamanaji hao walitoa mwito wa kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa haswa waliokamatwa katika maandamano, sanjari na kuwajibishwa waliohusika na mauaji ya waandamanaji.

Maandamano Sudan

Takwimu za madaktari zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu 83 wameuawa na mamia ya wengine wamejeruhiwa katika maandamano hayo ambayo yalianza Oktoba 25 mwaka jana, wakati jeshi lilipotangaza kutwaa madaraka kikamilifu nchini humo.

Maandamano hayo yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi mengine mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021 ambayo yaliiondoa madarakani serikali iliyokuwa inashirikisha pia raia nchini humo. 

Tags