Sierra Leone: Si haki Afrika kutowakilishwa katika Baraza la Usalama la UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81328-sierra_leone_si_haki_afrika_kutowakilishwa_katika_baraza_la_usalama_la_un
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone ametoa mwito wa kupewa nchi ya Kiafrika uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2022 04:30 UTC
  • Sierra Leone: Si haki Afrika kutowakilishwa katika Baraza la Usalama la UN

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone ametoa mwito wa kupewa nchi ya Kiafrika uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

David J. Francis ametoa mwito huo katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu, pambizoni mwa Jukwaa la Diplomasia la Antalya nchini Uturuki na kueleza kuwa, kwa miaka mingi sasa, Umoja wa Afrika umekuwa ukishinikiza kupatiwa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama bila mafanikio, jambo linaloashiria ukosefu wa haki na uadilifu wa kihistoria.

Ametoa mwito kwa viongozi wa dunia kuongoza mjadala wa kufanyiwa marekebisho Baraza la Usalama la UN akisisitiza kuwa, asilimia 75 ya mambo yanayojadiliwa kwenye taasisi hiyo yanalihusu bara Afrika, lakini kwa masikitiko hakuna nchi ya Kiafrika inayowakilishwa (ipasavyo) kwenye chombo hicho.

Amesema Umoja wa Afrika umeazimia kufanikisha ndoto yake hiyo, na tayari umeiteua Sierra Leone kuwa mwenyekiti wa kamati ya AU inayoshinikiza kufanyika mageuzi kwenye Baraza la Usalama. 

Tangu kuanzishwa kwa baraza hilo kwa zaidi ya miongo saba, bara la Afrika limesalia kuwa mshirika mdogo asiyekuwa na mchango muhimu katika mfumo wa utawala wa kimataifa. 

Viongozi wa Afrika wamekuwa wakipaza sauti mara kwa mara kulalamikia kile wanachokitaja kuwa kutokuweko uadilifu katika mfumo wa uongozi wa Baraza la Usalama na kupuuzwa bara la Afrika lenye nchi zaidi ya 50.

Nchi tano pekee za Marekani, China, Russia, Uingereza na Ufaransa zimeendelea kuwa nchi wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama ambazo zina haki ya kura ya turufu kwenye miswada na maamuzi ya baraza hilo.