Ecowas: Hatutaitelekeza Burkina Faso baada ya mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81548-ecowas_hatutaitelekeza_burkina_faso_baada_ya_mapinduzi
Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea kufanya kazi pamoja na Burkina Faso licha ya wasiwasi uliopo kuhusu mpango wa wanajeshi nchini humo kushikilia madaraka kwa miaka mitatu baada ya mapinduzi mwezi Januari mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 19, 2022 03:55 UTC
  • Ecowas: Hatutaitelekeza Burkina Faso baada ya mapinduzi

Mwakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea kufanya kazi pamoja na Burkina Faso licha ya wasiwasi uliopo kuhusu mpango wa wanajeshi nchini humo kushikilia madaraka kwa miaka mitatu baada ya mapinduzi mwezi Januari mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Shirley Ayorkor Botchway, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana ambaye aliyeongoza ujumbe wa Ecowas huko Ouagadougou mji mkuu wa Burkina Faso. Baada ya kuzungumza na kiongozi aliyesimamia mapinduzi huko Burkina Faso ambaye pia ni Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, Paul- Henri Damiba, Shirley amesema, matatizo na mashaka yanayoikumba Burkina Faso ni matatizo yao pia. Amesema, wakati huu ambapo Burkina Faso inahitaji msaada jumuiya ya Ecowas haiweza kuitelekeza na kuiacha pekee yake. 

Mjumbe wa Ecowas amesema kuwa walikuwa na  wasiwasi kuhusu kipindi cha miaka mitatu cha mpito kuelekea kurejeshwa demokrasia nchini Burkina Faso lakini uongozi wa kijeshi umeeleza hoja zake katika uwanja huo.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, jumuiya ya Ecowas ilisimamisha uanachama wa Burkina Faso ndani ya taasisi hiyo baada ya jeshi kumpindua aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Roch Kabore; hata hivyo haijaiwekea nchi hiyo vikwazo kama ilivyofanya kwa nchi jirani za Mali na Guinea ambazo pia zilikumbwa na mapinduzi ya kijeshi miezi 18 iliyopita. 

Roch Kabore, Rais wa Burkina Faso aliyepinduliwa na jeshi 

Katika mazungumzo ya Ouagadougou, Ecowas imetaka kuachiwa huru rais aliyepinduliwa Roch Kabore, ambaye amekuwa kizuizini kwa karibu miezi miwili sasa. Kiongozi wa wafanya mapinduzi nchini Burkina Faso aliuruhusu ujumbe wa Ecowas kumtembelea Kabore na amekutwa katika hali nzuri.