Maandamano ya Wasudani milioni moja kufanyika leo, wanapinga utawala wa kijeshi
Makundi yanayopinga utawala wa kijeshi nchini Sudan yameitisha maandamano ya watu milioni moja leo Jumatatu, ambayo wamesema yataelekea katika ikulu ya rais katikati mwa mji mkuu, Khartoum. Maandamano ya leo ya Wasudani yanafuatia yale yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika miji mingine kadhaa ya Sudan.
Makundi ya upinzani ya Khartoum mesema katika taarifa kwamba maandamano hayo ya Wasudani milioni moja yanafanyika chini ya kauli mbiu "kurejesha hadhi ya walimu," kuelekea Ikulu ya Rais."
Watayarisha wa maandamano hayo pia wamewataka wakazi wa miji ya Kassala (mashariki), Madani (kati) na Port Sudan (mashariki) kushiriki katika maandamano hayo.
Kwa upande wake, Jumuiya ya Walimu ya Sudan pia imekaribisha maandamano hayo ya watu milioni moja na kuthibitisha kwamba wanachama wake watashiriki.
Mji mkuu wa Sudan, Khartoum na mji wa Wad Madani, ulishuhudia maandamano jana Jumapili, yakitaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Shirika la Anadolu limewanukuu walioshuhudia wakisema kwamba makumi ya waandamanaji waliingia mitaani Jumapili jioni katika vitongoji kadhaa vya mji mkuu wa Sudan, Khartoum na Omdurman, wakitoa nara za kuitaka utawala wa kiraia.
Kwa miezi kadhaa sasa, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo kupinga utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao wamekuwa wakishinikiza kurejeshwa serikali ya kiraia nchini Sudan sambamba na kupinga utawala wa kijeshi tokea Oktoba 25 mwaka jana.