Sudan yakadhibisha madai ya kuwepo mamluki wa Russia nchini humo
Serikali ya Sudan imepuuzilia mbali madai ya Wamagharibi wanaodai kuwa, kuna mamluki wa Kundi la Wagner la Russia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekanusha vikali madai yaliyotolewa mabalozi wa Marekani, Uingereza na Norway kwamba harakati za wapiganaji hao wa Russia zinatatiza masuala ya ndani ya Sudan.
Wizara hiyo imesisitiza kuwa, madai ya kuwepo nchini humo mamluki wa 'Wagner Group' ya Russia hayana msingi wowote, na ni njama za mabalozi hao wa US, UK na Norway za kuiburuza Sudan katika mgogoro wa Ukraine.
Nchi hizo tatu za Magharibi zinazojiita Troika kwa ajili ya Sudan zilidai katika taarifa ya Machi 21 kuwa, mamluki wa Russia wa Kundi la Wagner wanafanya harakati zilizo kinyume cha sheria ili kudhalilisha utawala wa sheria wa Sudan.
Hata hivyo Khartoum kupitia Wizara ya Mashauri ya Kigeni imekadhibisha vikali madai hayo ya uwepo wa eti askari mamluki wa Russia katika nchi hiyo ya Kiafrika.
US, UK na Norway zilidai kuwa, Kundi la Wagner eti lenye mfungamano wa karibu na Rais Vladmir Putin wa Russia mbali na kueneza habari za kipropaganda kupitia mitandao ya kijamii, lakini pia linafanya uchimbaji haramu wa madini ya dhahabu.