Kuvunjwa Bunge la Tunisia
Rais Kais Saied wa Tunisia amelivunja Bunge la nchi hiyo kufuatia kushtadi mivutano ya kisiasa nchini humo.
Rais Kais Saied amechukua hatua hiyo baada ya zaidi ya wabunge 100 ambao shughuli zao zimesimamishwa kufanya mkutano kwa njia ya mtandao juzi Jumanne. Katika kikao hicho, wabunge zaidi ya 120 wa Tunisia walipiga kura wakiunga mkono kuondolewa hatua za dharura zilizotangazwa na Rais Saied.
Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Julai 25 mwaka jana. Rais wa nchi hiyo, Kais Saied wakati huo alichukua hatua za ghafla na kusitisha shughuli za Bunge na kisha akawafuta kazi Spika wa chombo hicho na Waziri Mkuu, Hicham Mechichi. Baada ya hapo kiongozi huyo alitwaa udhibiti wa masuala yote ya utendaji nchini humo. Kufutwa mamlaka ya Bunge, wabunge kuondolewa kinga, kuvunjwa jopo la kusimamia Katiba na kuvunja serikali na Baraza Kuu la Idara ya Mahakama ya nchi hiyo ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Rais Saied na kusababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa na matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vyama vya siasa nchini Tunisia vimezitaja hatua hizo za Kais Saied kuwa ni mapinduzi dhidi ya taasisi za serikali, Katiba ya nchi na dhidi ya mapinduzi ya wananchi yaliyouondoa madarakani utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali. Pamoja na hayo, Rais wa Tunisia anatilia mkazo kuwa ataendelea kutekeleza sera zake huku akiitaja hatua yoyote ya vyama vya kisiasa nchini humo kuwa ni jaribio la kufanya mapinduzi. Katika uwanja huo, Rais Kais amekitaja kikao cha wabunge kilichofanyika kwa njia ya mtandao kuwa ni jaribio lilifeli la mapinduzi na ametishia kuwafungulia mashtaka.

Rached Ghannouchi kiongozi wa chama cha Ennahda amezungumzia hilo akisema: "Kais Saied anataka Tunisia iwe nchi isiyo na chama cha siasa. Anataka kuwepo sauti moja tu ambayo ni sauti ya Rais wa nchi; rais ambaye anaongoza serikali peke yake na kuamua anachokitaka yeye. Rais huyohuyo ndiye anayepitisha sheria na kuzifuta na kukiuka Katiba. Anapindua Serikali na kuvunja Bunge ili kuhodhi kila kitu."

Wakati huo huo kupungua vigezo vyote vya uchumi wa Tunisia chini ya kivuli cha mgogoro wa sasa wa kisiasa nchini humo kunaonyesha kuwa nchi hiyo inakaribia kufilisika kiuchumi. Hali hiyo imezidisha pakubwa lawama na malalamiko ya wananchi wa Tunisia. Watunisia ambao baada ya vuguvugu la wananchi mwaka 2011 walitaraji kuboreka uchumi na hali ya kijamii sambamba na kurejea demokrasia nchini humo hivi sasa wana wasiwasi mkubwa wa kutofikiwa malengo waliyokusudia.
Harakati ya Ennahda ambayo ni moja ya vyama vikubwa katika siasa za Tunisia imetoa taarifa ikieleza kuwa: Rais Kais Saied anabeba dhima kutokana na kushindwa serikali yake iliyo kinyume cha sheria kutatua matatizo ya maisha ya watu wa Tunisia ikiwa pamoja na kupanda bei za bidhaa mbalimbali, uhaba mkubwa bidhaa muhimu pamoja na mashirika ya serikali kuwateuwa watu wasiofaa na wasio na ujuzi. Chama hicho kimetaka kufanyike mazungumzo yatakayovishirikisha vyama na makundi mbalimbali ya Tunisia ili kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo.
Inaonekana kuwa Tunisia inapita katika kipindi kigumu na si jambo lililo mbali kuona nchi hiyo ikirejea tena kwenye utawala wa kidikteta iwapo mwenendo huu utaendelea. Upande mmoja wa mgogoro huu ni Kais Saied, na upande mwingine ni vyama vya siasa na wananchi wa Tunisia ambao wana wasiwasi na mwenendo wa Kais Saied, kuzidi kudorora hali ya uchumi, kurejea udikteta na kupoteza malengo ya mapinduzi yao. Wakati huohuo baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu zinataka kuwa na ushawishi katika uga wa kisiasa na kiuchumi wa Tunisia kwa maslahi yao. Matamshi yaliyotolewa karibuni na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Abdulaziz bin Saud bin Nayef akiunga mkono serikali ya Kais Saied huko Tunisia ni ushahhidi wa ukweli huo
Inaonekana kuwa, mgogoro wa Tunisia utapamba moto katika siku zijazo sambamba na kuongezeka mivutano kati ya vyama, makundi mbalimbali na Rais Kais Saied kwa kuzingatia hatua iliyochukua kiongozi huyo ya kulivunja Bunge.