Ujumbe wa Israel wakutana na wakuu wa jeshi la Sudan mjini Khartoum
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya safari ya siri mjini Khartoum, na kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Sudan.
Shirika la habari la Kizayuni la Kan limenukuu duru za Sudan zikisema kuwa, maafisa wa Israel waliitembelea Khartoum mapema wiki hi, ambapo walikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa kijeshi wa Sudan.
Televisheni ya al-Arabiya ya Saudia imeripoti kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa intelijensia na usalama wa Israel wameandamana na maafisa kadhaa wa mamlaka za Israel kwenye safari hiyo.
Haya yanajiri wiki chache baada ya ujumbe mwingine wa Wazayuni kuitembelea Sudan na kukutana na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa kadhaa wa usalama na intelijensia wa Sudan wamekuwa wakiitembelea Tel Aviv pia, kwa kile kinachotajwa kuimarisha uhusiano wa kiusalama baina ya Sudan na utawala haramu wa Israel.
Mwishoni mwa mwaka 2020, na kwa upatanishi wa Marekani, Sudan na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia.
Hatua hiyo ilipingwa na kulalamikiwa vikali na wananchi na vyama vya siasa nchini Sudan, lakini watawala wa Khartoum hawakujali malalamiko hayo na wakaamua kuendeleza mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.