Euro bilioni 1.8 zakusanywa kwa ajili ya kupambana na njaa Afrika Magharibi
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, Euro bilioni 1.8 zimekusanywa kwa ajili ya kupambana na janga la njaa Afrika Magharibi.
Wataalamu wameonya kuwa, ukame mkali na janga la UVIKO-19 pamoja na mgogoro wa hivi sasa wa Ukraine kwa pamoja ni vitu ambavyo vimezidi kuifanya hali ya njaa kuwa mbaya sana katika eneo la Sahel na magharibi mwa Afrika.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema pia katika taarifa yake kuwa, Euro bilioni 1.8 zimekusanywa kwa ajili ya kuzisaidia nchi za ukanda huo kupambana na janga kubwa la njaa na kutahadharisha kuwa, kama hatua za haraka hazitochukuliwa, basi janga la njaa litawakumba watu milioni 30.3 wa ukanda huo ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
Mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kuwa, ukosefu wa chakula umesababishwa na kupanda kwa bei, vitendo vya kigaidi, mahitaji makubwa ya kikanda na janga la UVIKO-19. Mwakilishi wa WFP nchini Burkina Faso ameonya kwamba hali ni mbaya na mamilioni ya watu watakabiliwa na njaa mwaka huu.
Mkurugenzi mtendaji wa WFP, David Beasley amesema, idadi ya watu walioko katika hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa katika eneo la Sahel imeongezeka karibu mara kumi kwenye miaka mitatu iliyopita na idadi ya watu waliokimbia makazi yao imeongezeka kwa karibu asilimia 400 wakati eneo hilo likikabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa chakula kwa zaidi ya muongo mmoja.