Wahajiri 35 wahofiwa kufa maji Libya baada ya boti yao kupinduka
(last modified Sun, 17 Apr 2022 08:02:47 GMT )
Apr 17, 2022 08:02 UTC
  • Wahajiri 35 wahofiwa kufa maji Libya baada ya boti yao kupinduka

Umoja wa Mataifa umesema unahofia kuwa makumi ya wahajiri wameaga dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika Bahari ya Mediterrania, pwani ya Libya.

Shirika la Kimataifa la Wahajiri la Umoja wa Mataifa (IOM) liliripoti habari hiyo jana Jumamosi na kueleza kuwa, ajali hiyo ya boti ilitokea juzi Ijumaa katika mji wa Sabratha ulioko magharibi mwa Libya, moja ya vitovu vinavyotumiwa na wahajiri wanaotaka kwenda Ulaya kusaka maisha mazuri.

Taarifa ya IOM iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter imebainisha kuwa, miili sita imeopolewa baharini kufikia sasa, wahajiri wengine 29 waliotoweka wakihesabiwa kuwa wameaga dunia.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wahajiri wengine wanne kuthibitishwa kupoteza maisha baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama karibu na mji wa Surman, kaskazini magharibi mwa Libya.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM), tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, watu karibu 500 wamekufa maji wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya kinyume cha sheria.

Wahajiri karibu 3,000 walikufa maji baharini wakati wakijaribu kuelekea barani Ulaya kwa kutumia maeneo ya kaskazini mwa Afrika mwaka jana 2021.