Sudan yaitaka jamii ya kimataifa kuiwajibisha Israel baada ya kuvamia al Aqsa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imelaani vikali mashambulizi ya wanajeshi wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na shambulio dhidi ya waumini wa Kipalestina wasio na ulinzi waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Alfajiri katika eneo hilo.
Mapema Ijumaa iliyopita, wanajeshi wa Israel, wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni, walishambulia tena Msikiti wa Al-Aqsa na kuwajeruhi Wapalestina wasiopungua 160 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala. Wapalestina wengine 400 wametiwa nguvuni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan jana Jumapili ilitoa taarifa na kusisitiza kuwa, hatua kama hizo zinazozusha migogoro na za makusudi za utawala wa Kizayuni wa Israel zinaakisi hujuma ya wazi ya utawala huo dhidi ya utukufu ya Msikiti wa Al-Aqsa na heshima na nafasi yake katika dhamiri ya Umma wa Kiislamu, pamoja na ukiukaji wake wa wazi wa maazimio na mikataba ya kimataifa.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema, jamii ya kimataifa inapaswa kutekeleza wajibu wake na kuiwajibisha kikamilifu Israel kwa kuendelea kufanya jinai dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Palestina, ardhi yao na maeneo yao matakatifu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan pia imeitaka Israel kusitisha mashambulizi dhidi ya watu wa Palestina na juhudi zake za za Kuiyahudi Quds tukufu.
Katika taarifa hiyo, Sudan imesisitiza msimamo wake thabiti kuhusu haki ya watu wa Palestina ya kujiamulia hatima yao na kuanzisha nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas.
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alikuwa ameitaka jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la umoja huo kuilaani Israel kwa mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina na hatua zake za mara kwa mara za kuyavunjia heshima maeneo matakatifu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.