UN: Hali ya watu wa Darfur inatia wasiwasi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa makumi ya maelfu ya raia waliokimbia mapigano makali yanayoendelea kati ya jeshi la serikali ya Sudan na waasi wa eneo la Jabal al Murrah huko magharibi mwa Darfur wanaishi katika hali inayovunja moyo na kuhuzunisha.
Vita katika eneo hilo la milimani vilianza tarehe 15 Januari baina ya askari watiifu kwa Rais Omar al Bashir wa Sudan na waasi wa SPLA tawi la Abdul Wahiid Nour.
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Marta Ruedas, amesema kuwa machafuko hayo yamesababisha wimbi kubwa la wakimbizi ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo hilo kwenye muongo mmoja uliopita.
Ofisi ya Mratibu Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa, karibu watu elfu 38 yumkini wamekimbia eneo la Darfur Kaskazini. Imeongeza kuwa, tathmini ya idadi ya wakimbizi huko Darfur ya Kati inatatiza na kwamba kuna uwezekano idadi ya wakimbizi katika eneo hilo inafikia elfu 50.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa, watu zaidi ya laki tatu wameuawa katika machafuko ya Darfur yaliyoanza mwaka 2003 na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi.