Viongozi wa Sudan wapiga marufuku maandamano ya aina yoyote
(last modified Sat, 30 Apr 2022 11:25:02 GMT )
Apr 30, 2022 11:25 UTC
  • Viongozi wa Sudan wapiga marufuku maandamano ya aina yoyote

Viongozi wa Sudan wametangaza kupiga marufuku maandamano yoyote yale kwa mnasaba wa miaka mitatu ya maandamano ya kulalamikia madaraka ya nchi kutwaliwa na wanajeshi wa nchi hiyo.

Taarifa hiyo ya serikali imefuatia tangazo la Kamati ya Muqawama mjini Khartoum ambayo leo ilitangaza kuitisha maandamano katika mji mkuu huo.

Kamati ya Usalama ya Sudan imesisitiza kuuwa, ni marufuku kufanya maandamano au mikusanyiko yenye lengo la kulalamikia utawala ulioko madarakani.

Hata hivyo wapinzani nchini Sudan wamesisitiza kuwa, utawala ulioko madarakani unapaswa kuruhusu kufanyika maandamano kwani hiyo ni haki yao kikatiba.

Mamlaka husika Sudan zinasisitiza kwamba, maandamano yoyote yanapaswa kufanyika kwa uratibu na vyombo vya usalama na kwamba, ni marufuku kufanya mikusanyiko au maandamano katika maeneo ya karibu na hospitali na taasisi za elimu.

Maandamano ya wananchi wa Sudan ya kupinga utawala wa kijeshi

 

Kwa miezi kadhaa sasa, wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo kupinga utawala wa majenerali wa kijeshi ambao ni vibaraka wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa, uwepo wa jeshi kwenye madaraka ni kinyume na malengo yao yaliyopelekea kuondolewa madarakani rais wa zamani Omar al-Bashir. Wasudani wanataka kuondoka madarakani kikamilifu jeshi la nchi hiyo na kuanzishwa serikali halali na ya kidemokrasia, lakini maafisa wa jeshi hawako tayari kuondoka madarakani.

Tags