May 17, 2022 07:36 UTC
  •  Mahakama Jamhuri ya Afrika ya Kati yaanza kusikiliza kesi ya kwanza ya jinai za kivita

Mahakama Inayoendesha Kesi za Uhalifu wa Kivita nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati imeanza kusikiliza kesi ya kwanza ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na jinai za kivita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Kikao cha kwanza cha Mahakama Kuu ya Uhalifu Afrika ya Kati kilifanyika kusikiliza kesi ya watuhumiwa wa uhalifu wa kivita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa ni nchi ya pili yenye ustawi duni duniani inaendelea kuathiriwa na hali ya mchafukoge na vita vya ndani tokea mwaka 2013 alipoondolewa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize. Makundi yanayobeba silaha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yanadhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo.  

Francois Bozize, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyepinduliwa 

Watu wanaotuhumiwa kuhusika na jinai mbalimbali za kivita katika mizozo na machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mara ya kwanza wamefikishwa mahakamani  miaka saba baada ya kuanzishwa mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita nchini humo. 

Issa Sallet Adoum, Ousman Yaouba na Tahir Mahamat ni kati ya wanachama wa kundi la kigaidi lenye nguvu la nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.  

Watu hao wanatuhumiwa kwamba, tarehe 21 Mei mwaka 2019 waliwauwa kwa umati raia 56 katika vijiji mbalimbali katika maeneo ya Lemouna na Koundjili kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.  

Mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita ilianza kuchunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na jinai za kivita huko Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2018.

 

Tags