DRC yaituhumu Rwanda kuwa imetuma mamia ya askari nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i84568-drc_yaituhumu_rwanda_kuwa_imetuma_mamia_ya_askari_nchini_humo
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limedai kuwa Rwanda imetuma mamia ya askari ndani ya ardhi ya nchi hiyo, huku wasiwasi na taharuki ikiendelea kushuhudiwa kati ya nchi hizo jirani na kutishia uhusiano baina yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2022 18:51 UTC
  • DRC yaituhumu Rwanda kuwa imetuma mamia ya askari nchini humo

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limedai kuwa Rwanda imetuma mamia ya askari ndani ya ardhi ya nchi hiyo, huku wasiwasi na taharuki ikiendelea kushuhudiwa kati ya nchi hizo jirani na kutishia uhusiano baina yao.

Jeshi la DRC limesema katika taarifa kuwa, wanajeshi 500 wa Rwanda wametumwa katika eneo la Tshanzu katika mkoa wa Kivu Kaskazini mpakani mwa nchi mbili hizo; madai ambayo serikali ya Kigali imeyakanusha na kuyatupilia mbali.

Taarifa ya Jeshi la Kongo DR imeeleza kuwa, wanajeshi wa Rwanda waliotumwa nchini humo wamevalia magwanda yenye rangi za kijani na nyeusi, tofauti na sare rasmi za jeshi la Rwanda.

Haya yanajiri wiki moja baada ya Rwanda kuonya kuwa, itajibu mapigo endapo itashambuliwa tena na jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mgogoro wa kidiplomasia baina ya Kigali na Kinshasa umeongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya pande zote mbili kutuhumiana kuwa zinaunga mkono waasi mashariki mwa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linalopakana na Rwanda.

Wanajeshi wa Rwanda wakiwa wamevalia sare rasmi

Serikali ya Kinshasa inaituhumu Kigali kuwa inawaunga mkono waasi wa Kitutsi wa M23 ambao wamekuwa wakitekeleza mauaji ya kinyama huko mashariki mwa DRC.

Katika upande wa pili Rwanda inaituhumu DRC kuwa inawaunga mkono waasi wa Kihutu wa FDLR. Nchi zote mbili zimekanusha madai ya kuwaunga mkono waasi.