UN: Mauaji mapya ya kikabila nchini Sudan yameua watu 145
(last modified Wed, 15 Jun 2022 11:49:57 GMT )
Jun 15, 2022 11:49 UTC
  • UN: Mauaji mapya ya kikabila nchini Sudan yameua watu 145

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu waliouawa katika wimbi jipya la mapigano ya kikabila huko Sudan imeongezeka na kufikia 145.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mapigano ya kikabila yaliyosababisha mauaji hayo yameripotiwa katika mikoa ya Darfur Magharibi na Kordofan Kusini.

OCHA imesema mbali na watu 145 kuuawa katika mapigano hayo mapya yaliyoanza mapema mwezi huu, wengine zaidi ya 180 wamejeruhiwa.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, vijiji 25 katika eneo la Kulbus vimeshambuliwa kwa kuchomwa moto na kuibiwa kwenye mapigano hayo, na kupelekea watu 50,000 kuyakimbia makazi yao.

Ripoti ya OCHA imesema tangu mwanzoni mwa mwezi huu hadi sasa, watu 126 wakiwemo 101 wa kabila la Gimir na Waarabu 25 wa jamii ya Rizeigat wameuawa, katika mkoa wa Darfur Magharibi na mkoa jirani wa Darfur Kaskazini.

Vijiji vilivyochomwa moto Darfur

Aidha watu 19 wameuawa mpaka sasa katika mapigano mengine tofauti ya kikabila katika mkoa wa Kordofan Kusini, mbali na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.

Machafuko hayo yanaripotiwa huku Sudan ikiwa imegubikwa na wimbi la machafuko yaliyosababishwa na mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka uliopita yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Tags