UN: Thuluthi moja ya Wasudan wanakabiliwa na njaa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema zaidi ya asilimia 30 ya wananchi wa Sudan wanasumbuliwa na mgogoro mkubwa wa chakula uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, mzozo wa kisiasa na kupanda bei za chakula katika soko la dunia.
Taarifa ya pamoja ya Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo la umoja huo (FAO) imesema watu milioni 15 wanakabiliwa na ukosefu wa usalama chakula katika mikoa yote 18 ya nchi hiyo ya Kiarabu, mashariki mwa Afrika.
Eddie Rowe, mwakilishi wa WFP nchini Sudan amesema: Athari za mgogoro wa hali ya hewa, migogoro ya kiuchumi na kisiasa, kupanda bei za vyakula na kutopatikana mavuno ya kutosha kumewatumbukiza mamilioni ya watu katika njaa na umaskini.
Ripoti hiyo imesema asilimia 40 ya Wasudan watatumbukia katika mgogoro mkubwa wa chakula kufikia Septemba mwaka huu, iwapo taifa hilo halitapewa misaada ya dharura ya kibinadamu.
Katika hatua nyingine, taarifa ya pamoja na mashirika ya Plan International, Save the Children na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa imeonya kuwa, watoto 375,000 wa Sudan wenye chini ya miaka 5 na wanaosumbuliwa na utapiamlo huenda wakapoteza maisha mwaka huu iwapo hawatapatiwa matibabu.
Mbali na migogoro ya kimaumbile na mizozo ya kisiasa, Sudan pia inasumbuliwa na mapigano na mauaji kikabila hususan katika mikoa ya Darfur Magharibi na Kordofan Kusini.