Niger wafanya maandamano kulaani jinai za Boko Haram
Wananchi wa mji mkuu wa Niger, wamefanya maandamano makubwa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni ya genge la kigaidi la Boko Haram.
Redio ya Kimataifa ya Ufaransa imetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, makumi ya wakazi wa Niamey wameandamana mjini humo kulaani jinai za kundi la kigaidi la Boko Haram.
Jumuia za kijamii za Niger, vyama vya wafanyakazi na wanasiasa mashuhuri ni miongoni mwa walioshiriki kwenye maandamano hayo.
Mwakilishi mmoja wa jumuia za kijamii nchini Niger ameitaka serikali ya nchi hiyo kutumia uwezo wake wote kuhakikisha inalimaliza kabisa kundi la Boko Haram nchini humo.
Ikumbukwe kuwa, shambulio la kwanza kabisa la Boko Haram katika nchi jirani ya Niger lilifanyika mwezi Februari mwaka jana. Kabla ya hapo mashambulizi ya kundi hilo yalikuwa yanafanyika nchini Nigeria tu.
Katika shambulio la karibu kabisa la siku ya Ijumaa, wanamgambo wa Boko Haram walivamia kambi ya kijeshi ya Niger katika eneo la mpakani la Bosso la kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuua wanajeshi 30 wa Niger na wanajeshi wawili wa Nigeria na kujeruhi wengine 67.