Tisa wauawa Sudan katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi
Takriban waandamanaji tisa waliuawa kwa kupigwa risasi nchini Sudan siku ya Alhamisi, matabibu wamesema, huku umati mkubwa wa watu ukiingia mitaani licha ya ulinzi mkali na kukatika kwa mawasiliano kuandamana dhidi ya utawala wa kijeshi ulionyakua mamlaka miezi minane iliyopita.
Katikati ya Khartoum, vikosi vya usalama vilifyatua gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji kuandamana kuelekea ikulu ya rais.
Inakadiriwa umati wa watu mjini Khartoum na miji yake pacha ya Omdurman na Bahri ilifika makumi ya maelfu na hivyo kuyafanya maandamano ya jana kuwa makubwa zaidi katika miezi ya karibuni. Huko Omdurman, mashahidi waliripoti gesi ya kutoa machozi na milio ya risasi huku vikosi vya usalama vikiwazuia waandamanaji kuvuka hadi Khartoum, ingawa baadhi yao walivuka baadaye.
Maandamano hayo katika mji mkuu na miji mingine yameadhimisha mwaka wa tatu wa maandamano makubwa wakati wa vuguvugu lililompindua mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir na baada ya kupinduliwa al Bashir kulizinduliwa mpango wa kugawana madaraka kati ya makundi ya kiraia na wanajeshi.
Oktoba mwaka jana, jeshi likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan liliipindua serikali ya mpito, na kusababisha maandamano ya kutaka jeshi liache siasa.
Juni 30 pia inaadhimisha siku ambayo Bashir alichukua mamlaka katika mapinduzi mwaka 1989.
Ilikuwa ni mara ya kwanza katika miezi kadhaa ya maandamano kwamba huduma za mtandao na simu zilikatwa. Baada ya jeshi kuchukua mamlaka, kukatika kwa mtandao kwa muda mrefu kuliwekwa katika juhudi za kudhoofisha harakati za maandamano.
Vifo tisa vya Alhamisi, sabaa vilivyotokea Omdurman, kimoja Khartoum na mtoto mwingine huko Bahri vilifikisha idadi ya waandamanaji waliouawa tangu mapinduzi hayo kufikia 111. Kulikuwa na majeruhi wengi na majaribio ya vikosi vya usalama kuvamia hospitali za Khartoum ambako walikuwa wakitibiwa.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, alitoa wito wiki hii kwa mamlaka kutii ahadi ya kulinda haki ya kukusanyika kwa amani.