ADF yashambulia kliniki na kuua watu 13 mashariki ya DRC
(last modified Sat, 09 Jul 2022 07:37:47 GMT )
Jul 09, 2022 07:37 UTC
  • ADF yashambulia kliniki na kuua watu 13 mashariki ya DRC

Kwa akali watu 13 wameuawa katika shambulizi jipya la waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jeshi la DRC lilitangaza habari hiyo jana Ijumaa na kueleza kuwa, wanamgambo hao wa ADF waliua wagonjwa tisa kwenye kituo hicho cha afya Alkhamisi usiku.

Kasereka Ise Mighambo, Meya wa mji wa Lume katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema waasi hao wa ADF waliua wagonjwa wanne ndani ya kliniki hiyo, na raia wengine tisa kabla ya kutorokea katika Hifadhi ya Virunga.

Ameeleza kuwa, wagonjwa wawili wameuawa kwa kuchomwa moto na wapiganaji hao, ambao pia walikiteketeza kwa moto kituo hicho cha kutoa matibabu. 

Waasi wa ADF

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Vikosi vya Jeshi la Uganda (UPDF) na  Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vilianzisha mashambulizi mwaka jana ili kuwaondoa waasi hao wa ADF, ambao wamekuwa wakiwashambulia na kuwaua raia mashariki kwa zaidi ya miongo miwili.

 

Tags