Genge la ADF laendeleza wimbi la umwagaji damu DRC
(last modified Mon, 11 Jul 2022 11:22:45 GMT )
Jul 11, 2022 11:22 UTC
  • Genge la ADF laendeleza wimbi la umwagaji damu DRC

Watoto wanne ni miongoni mwa watu watano waliouawa katika shambulizi jipya la waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jacques Anayeyi, kiongozi wa Baraza la Vijana katika mkoa wa Ituri, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, watu waosadikiwa kuwa wa wapiganaji wa ADF usiku wa kuamkia jana walishambulia kijiji cha Busiyo na kuteketeza moto nyumba kadhaa.

Ameongeza kuwa, mbali watu watano kuuawa na watano kujeruhiwa katika hujuma hiyo, lakini makumi ya wengine wameshikwa mateka na genge hilo.

Shambulio hilo la Jumamosi usiku limejiri siku mbili tu baada ya watu wengine 13 kuuawa katika hujuma ya waasi wa kundi la ADF dhidi ya kituo cha matibabu katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Waasi wa ADF

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Vikosi vya Jeshi la Uganda (UPDF) na  Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vilianzisha mashambulizi mwaka jana ili kuwafurusha waasi hao wa ADF, ambao wamekuwa wakiwashambulia na kuwaua raia mashariki kwa zaidi ya miongo miwili.

Tags