Rais wa Ivory Coast atoa msamaha kwa mtangulizi wake, Laurent Gbagbo
(last modified Sun, 07 Aug 2022 12:36:40 GMT )
Aug 07, 2022 12:36 UTC
  • Rais wa Ivory Coast atoa msamaha kwa mtangulizi wake, Laurent Gbagbo

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast ametoa msamaha kwa mtangulizi wake, mshindani wake mkuu na hasimu wake wa muda mrefu Laurent Gbagbo, ikiwa ni sehemu ya kuleta maridhiano nchini kuelekea uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika 2025.

Ouattara ametoa tangazo hilo la msamaha Jumamosi kupitia televisheni ya taifa, siku moja kabla ya sherehe za uhuru wa Ivory Coast zinazofanyika leo.

“Kwa faida ya kuimarisha mshikamano wa kijamii, nimesaini dikrii ya kutoa msamaha wa urais”, ameeleza Rais Ouattara katika sehemu ya tangazo hilo.

Rais wa Ivory amebainisha pia kuwa ameagiza akaunti za benki za Gbagbo zilizokuwa zimefungwa zifunguliwe na aanze kupatiwa malipo ya ustaafu wa urais ya kudumu hadi mwisho wa uhai wake.

Laurent Gbagbo aliyekuwa rais wa Ivory Coast kuanzia mwaka 2000 hadi 2011 alirudi nchini humo 2019 baada ya kufutiwa mashtaka na Mahakama ya Kimataifa Jinai (ICC) iliyoko the Hague ya kuhusika na jinai za kivita kwa kuhusika kwake katika vita vya ndani vilivyochochewa na msimamo wake wa kutokubali matokeo ya kura yaliyoonyesha kuwa alishindwa katika uchaguzi wa rais wa Ivory Coast wa mwaka 2010.

Gbagbo aliposhtakiwa ICC

 

Uamuzi wa Rais Ouattara wa kutoa msamaha huo, unafuatia mkutano wa aina yake uliofanyika mwezi uliopita wa Julai baina yake, Gbabgo pamoja na rais mwingine wa zamani wa Ivory Coast Henri Konan Bedie.

Viongozi hao watatu ndio waliotawala uga wa mirengo ya kisiasa ya Ivory Coast tangu muongo wa 1990.

Gbagbo na Bedie wamealikwa pia kuhudhuria sherehe za uhuru zinazofanyika leo katika mji mkuu wa kisiasa wa nchi hiyo Yamoussoukro…/