Mali: Wanajeshi wa Ivory Coast waliotuhumiwa kuwa 'mamluki' wameshtakiwa na kufungwa
Duru za mahakama nchini Mali zimeripoti kuwa, wanajeshi 49 wa Ivory Coast waliozuiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika mji mkuu Bamako, wakishutumiwa na jeshi lililoko madarakani nchini Mali kwa kuwa "mamluki", madai ambayo serikali ya Abidjan inakanusha, wameshtakiwa kwa "kujaribu kuhatarisha usalama wa taifa" na kuhukumiwa kifungo jela.
Hayo yamethibitishwa na Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Mali.
Afisa wa wizara ya sheria ya Mali amevidokeza vyombo vya habari akisema: "askari hao 49 wamefunguliwa mashtaka na kuwekwa chini ya hati ya kukamatwa kwa ''kuhatarisha usalama wa taifa'' na sababu zingine".
Serikali ya Ivory Coast inasisitiza kuwa, wanajeshi hao waliokamatwa nchini Mali walikuwa kwenye utekelezaji kazi za kikosi cha Umoja wa Mataifa, kama sehemu ya operesheni za usaidizi wa vifaa kwa Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) na inaomba wanajeshi hao waachiliwe huru.
Askari wao wa jeshi la Ivory Coast walikamatwa Julai 10 walipowasili katika uwanja wa ndege wa Bamako.
Tukio la kukamatwa na kushtakiwa wanajeshi wa Ivory Coast linachukuliwa kama mwendelezo wa mvutano kati ya nchi hiyo na Mali ambayo inaituhumu Abidjan kuwa iliwashawishi washirika wake wa Afrika Magharibi kuimarisha vikwazo dhidi ya wanajeshi wa Mali ambao wamefanya mapinduzi mawili tangu mwaka 2020, vikwazo ambavyo viliondolewa mapema mwezi wa Julai.
Togo imekabidhiwa jukumu la upatanishi kati ya Mali na Ivory Coast ili kuwezesha kuachiwa huru wanajeshi hao, lakini mazungumzo ya awali yaliyofanyika mjini Lome Julai 28 hayakuzaa matunda.../