Raia 100 watekwa nyara na wanamgambo kaskazini mwa Kongo DR
Viongozi wa kieneo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wameonyesha wasi wasi wao juu ya hatma ya raia 100 waliotekwa nyara na wanamgambo huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na viongozi hao wa kieneo imesema kuwa, hivi karibuni wanamgambo wa Uganda walishambulia kijiji cha Gumbu, kilichopo katika mkoa wa Bas-Uélé, kaskazini mwa nchi hiyo na kuwateka nyara mamia ya raia wa kijiji hicho na kwenda nao kusikojulikana. Kwa mujibu wa viongozi hao wa kieneo, wanamgambo waliofanya shambulizi hilo, wilikuwa 50 na kwamba awali walianza kuvamia maduka na makazi ya raia na kupora vitu mbalimbali. Wamesisitiza kuwa, ili kubeba vitu hivyo vilivyoporwa, waliamua kuwateka nyara watu hao na kutoweka nao hadi leo. Polisi wa serikali wameanzisha operesheni za kufuatilia nyendo za wanamgambo hao ingawa hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusiana nao.