Ukame watishia maisha ya watu na mifugo Somalia, UN yaonya
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu ametahadharisha kuhusu kutokea janga kubwa la kibinadamu kutokana na ukame wa muda mrefu katika maeneo tofauti ya Somalia.
Martin Griffiths alitoa tahadhari hiyo jana (Jumatatu) huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia na kuongeza kuwa, takwimu za karibu kabisa zinoenesha kuwa, katika kipindi cha baina ya mwezi Oktoba hadi Disemba 2022, maeneo mawili ya Baidoa na Buur Hakaba ya kusini mwa Somalia yatakumbwa na ukame mkubwa.
Akiwa ziarani nchini Somalia, Griffiths ametembelea maeneo tofauti yakiwemo ya Baidoa na kuona kwa karibu hali ya watoto katika eneo hilo ambao wameathiriwa vibaya na lishe duni. Akiwa katika eneo hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema, nimepigwa na bumbuwazi baada ya kuona hali mbaya ya wananchi wa Baidoa hususan watoto na jinsi wanavyohimili mashaka na matatizo mengi ambayo ni vigumu kubebeka.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa pia amesema, inakadiriwa kuwa hali hiyo mbaya ya wananchi wa Baidoa itaendelea hadi mwezi Machi 2023.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, watu milioni 7 na 800,000 ambao wanaunda nusu nzima ya wananchi wote wa Somalia wanateseka kwa njaa kutokana na ukame huku watu 2,13,000 kati yao wakiwa katika hali mbaya zaidi.
Tangu mwaka 2021 hadi hivi sasa, njaa na ukame umewaathiri vibaya watu wasiopungua milioni moja katika kona mbalimbali za Somalia.
Ingawa kwa muongo mzima sasa Somalia imo katika ukame na ukosefu wa mvua lakini ukame wa hivi sasa ni mbaya zaidi uliko wa miaka ya 2010-2011 na 2016-2017.