Chad yatuma maelfu ya wanajeshi Niger
Chad yatuma wanajeshi elfu mbili nchini Niger iili kukabiliana na mashambulizi ya Boko Haram.
Duru za kijeshi za Chad zimearifu kuwa jeshi la nchi hiyo limetuma wanajeshi elfu mbili kuelekea Niger, nchi ambayo Ijumaa iliyopita ilikumbwa na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Wanajeshi 30 wa Niger na 2 wa Nigeria waliuawa katika shambulio lililotekelezwa Ijumaa iliyopita na kundi la kigaidi la Boko Haram katika kituo kimoja cha kijeshi katika eneo la Bosso kusini mashariki mwa Niger. Watu wengine 67 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Duru za kijeshi za Chad zimeongeza kuwa, wanajeshi hao wa Chad huku wakiwa na silaha nyingi, Jumatatu wiki hii walielekea katika mpaka wa Niger na Chad ili kukabiliana na mashambulizi ya Boko Haram. Maeneo ya Bosso na Diffa yanayopatikana kusini mashariki mwa Niger na vile vile maeneo mengine ya Niger yenye mpaka wa pamoja na Nigeria, tangu mwezi Februari mwaka jana hadi sasa yamekuwa yakikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram. Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi barani Afrika kutokana na mashambulizi na vitendo vya kigaidi vya Boko Haram tangu mwaka 2009 hadi sasa.