Alkhamisi, tarehe 3 Agosti, mwaka 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria sawa na tarehe 3 Agosti mwaka 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 531 iliyopita baharia wa Kiitalia Christopher Columbus alianza safari kubwa zaidi ya kiuvumbuzi. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya inayoelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania. Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Baharia huyo wa Kiitalia na wenzake walidhani kuwa wamefika India. Hata hivyo walikuwa wamefika katika kisiwa kilichojulikana kwa jina la Salvador katika bara la Amerika.
Miaka 109 iliyopita katika siku kama hii ya leo Mfereji wa Panama ulifunguliwa baada ya meli ya kwanza kupita katika mfereji huo. Mfereji wa Panama ulianza kujengwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye ujenzi huo ukakamilishwa na Wamarekani. Mfereji wa Panana ulio na urefu wa kilomita 68 unaunganisha bahari mbili za Atlantic na Pacific. *
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, mwafaka na tarehe 3 Agosti 1960, nchi ya Kiafrika ya Niger ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Niger ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa tangu karne ya 18 na mwaka 1922 ikawa koloni rasmi la Wafaransa baada ya nchi hiyo kujenga vituo vyake vya kijeshi nchini humo. Hata hivyo taratibu wananchi wa Niger walianzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na hatimaye nchi hiyo ilifanikiwa kupatia uhuru katika siku kama hii ya leo. Niger iko magharibi mwa Afrika na inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, MOSSAD, katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel. *