Hali ya mchafukoge yashuhudiwa Congo DR kutokana na uhaba wa mafuta
(last modified Fri, 09 Sep 2022 10:15:43 GMT )
Sep 09, 2022 10:15 UTC
  • Hali ya mchafukoge yashuhudiwa Congo DR kutokana na uhaba wa mafuta

Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, uhaba wa mafuta umezusha hali ya mchafukoge na ukosefu wa nidhamu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.

Vita vya Ukraine vimesababisha uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu hususan nishati ya mafuta na gesi na kupelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa hizo.

Ripoti zinasema, safu ndefu za magari zimeshuhudiwa mjini Kinshasa hususan karibu na vituo vya mafuta ya pertoli, suala ambalo limesababisha msongamano mkubwa wa magari katika jiji la Kinshasa linalosumbuliwa na uhaba mkubwa wa mafuta kwa siku kadhaa sasa.

Tangu Jumatatu iliyopita, mafuta ya petroli yameadimika mjini Kinshasa kwa sababu ambazo serikali haijaziweka wazi, na vituo vya mafuta katika mji huo mkubwa wenye watu wapatao milioni 15 vinafungwa hatua kwa hatua.

Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kwamba kuna upungufu mkubwa wa akiba ya mafuta nchini humo na imewalazimisha wasambazaji wa nishati kuuza mafuta ya petroli kwa mgao.

Waziri wa Nishat wa Congo DR pia amewataka wakazi wa mji wa Kinshasa kubana matumizi ya nishati na mafuta.

Kwa mujibu wa mgao wa sasa, madereva wa magari ya watu binafsi wanapewa lita 20 za petroli na mabasi ya umma yanaruhusiwa kununua mafuta yasiyozidi lita 30. Hata hivyo mafuta yameadimika kabisa mjini Kinshasa na magari ya usafirishaji wa umma yameonekana katika safu ndefu katika maeneo ya kandokando ya vituo vya petroli.

Tags