IGAD: Malaki ya watu katika hatari ya kufa njaa Afrika Mashariki
Mamia ya maelfu ya watu wapo katika hatari ya kufariki dunia kutokana na baa la njaa lililozikumba nchi za kanda ya Afrika Mashariki.
Hayo ni kwa mujibu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na Pembe ya Afrika IGAD ambayo imeongeza kuwa, watoto zaidi ya milioni 10 katika eneo hilo wanasumbuliwa na utapiamlo.
Workneh Gebeyehu, Katibu Mkuu wa IGAD amesema eneo la Afrika Mashariki linakabiliwa na kipindi kirefu zaidi cha ukame ndani ya miaka 4, huku likikabiliwa na ukame kwa mara ya nne ndani ya muongo mmoja.
Amesema watoto zaidi ya milioni 10 katika nchi sita wanachama wa IGAD wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu. Nchi wanachama wa IGAD ni Djibouti, Ethiopia, Somalia, Eritrea, Sudan, Sudan Kusini, Kenya, na Uganda.
Zaidi ya raia millioni 20 kutoka mataifa ya Kenya, Somalia, Ethiopia na Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu na ukosefu wa mvua za kutosha.
Takwimu za IGAD zinaonesha kuwa, watu milioni 51 katika nchi saba za IGAD wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, wakiwemo 388,000 ambao wapo katika hatari ya kufa njaa.