SADC: Watu milioni 68 wanasumbuliwa na ukame kusini mwa Afrika
(last modified Sun, 18 Aug 2024 07:02:22 GMT )
Aug 18, 2024 07:02 UTC
  • SADC: Watu milioni 68 wanasumbuliwa na ukame kusini mwa Afrika

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema makumi ya mamilioni ya watu wameathiriwa na ukame uliosababishwa na El Nino katika eneo la Kusini mwa Afrika, na wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.

Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi aliuambia mkutano huo wa 44 wa SADC jana Jumamosi katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare kwamba, watu milioni 68 (17% ya wakazi wa eneo hilo), wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Ukame huo umeharibu sana mazao ya eneo hilo, huku ombi la kibinadamu la dola bilioni 5.5 likizinduliwa mwezi Mei, kutafuta usaidizi wa kukabiliana na athari za ukame.

Mbali na kufanya mamilioni wahitaji msaada wa dharura wa chakula, madhara mengine ya ukame huo ni pamoja na uhaba mkubwa wa nishati, huku nchi kama Zambia, ambayo imetangaza ukame kuwa janga la kitaifa, zikitarajia kuagiza bidhaa kutoka mataifa jirani ili kukwamua chumi zao.

Februari mwaka huu, kiangazi kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, kiliripotiwa katika nchi za Zambia na Zimbabwe, huku Malawi, Msumbiji na sehemu za Angola zikiwa na "upungufu mkubwa wa mvua."

Marais na wakuu wa jumuiya ya SADC

Mwenyekiti wa zamani wa SADC, Joao Lourenco, Rais wa Angola ambaye amekabidhi jukumu hilo kwa Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema, mengi bado yanahitajika kufanywa ili kukusanya pamoja rasilimali kwa lengo la kusaidia mataifa yaliyoathirika.

Mkutano huo ambao ulikwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya SADC, ulifanyika chini ya kaulimbiu, 'Kukuza ubunifu ili kufungua fursa za ukuaji endelevu wa uchumi na maendeleo kuelekea SADC yenye viwanda.'