Nov 30, 2023 03:49 UTC
  • Ukame kulazimisha watu milioni 216 duniani kuyahama makazi yao

Inakadiriwa kuwa, watu milioni 216 watalazimika kuyahama makazi yao kufikia mwaka 2050 kutoka na athari za ukame.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti hayo na kuongeza kuwa, maeneo ya dunia ambayo yataathirika zaidi na athari za ukame ni maeneo yanayozunguka Bahari ya Mediterrania, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, watu milioni 55 huathiriwa moja kwa moja na makali ya ukame katika pembe zote za dunia. Kwa ujumla, watu bilioni 1.4 waliathiriwa na ukame kote duniani baina ya mwaka 2000 na 2019.

Inakadiriwa kuwa, watu baina ya milioni 500 na 600 watahama makazi yao na kuelekea upande wa kaskazini kutoka na taathira hasi za ukame katika nchi za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati.  

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni 81 barani Afrika wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na ukame. Joto kali na ukame vimezifanya nchi nyingi za bara hilo zikabiliwe na njaa isiyo na kifani.

Ukame Somalia

Somalia ambayo hivi sasa inasumbuliwa na mafuriko, ni moja ya nchi zilizoathiriwa zaidi na taathira za ukame. Kwa mujibu wa shirika la kibinadamu la Islamic Relief,  watu milioni 4.3 wamehama makazi yao katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kutokana na ukame na ukosefu wa usalama. Aidha malaki ya wengine wahama makazi yao kutokana na mafuriko.

Habari zaidi zinasema kuwa, jumla ya Wakenya milioni 4.35 wameathiriwa na ukame ambapo kati yao kuna watoto 960,000 ambao wana utapiamlo na wana uhitaji mkubwa wa chakula. Nchi hiyo pia kama vile Ethiopia, hivi sasa inasumbuliwa na mafuriko kutokana na mvua za el-Nino.

Tags