Baqaei: Mashinikizo ya kisiasa hayawezi kudhoofisha haki ya Iran ya kurutubisha urani
-
Ismail Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa haki "isiyoweza kubatilishwa" ya Iran ya kurutubisha madini ya urani haiwezi kudhoofishwa na mashinikizo ya kisiasa.
Ismail Baqaei amesema kuwa haki ya Iran na kutumia kwa amani na kwa malengo ya kiraia nishati ya nyuklia ni ya asili na isiyoweza kuondolewa, na hakuna aina yoyote ya mashinikizo au msimamo wa kisiasa unaoweza kudhoofisha haki hiyo.
"Kifungu cha IV (nne) cha Mkataba wa Kuzuia Uenezi na Usambazaji za Silaha za Nyuklia (NPT) kinatambua haki ya nchi zote zilizotia saini mkataba huo kwa ajili ya matumizi ya kiraia ya nishati ya nyuklia", amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Baqaei ameongeza kuwa, tangu Iran ulipoidhinisha mkataba wa NPT mwaka 1970, Tehran imeheshimu majukumu yake na, kwa msingi huo imezingatia kunufaika na haki zilizoainishwa katika mkataba huo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hata hivyo tafsiri za upande mmoja na za kisiasa za mataifa fulani yenye silaha za nyuklia zimetilia shaka hata matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.
Iran ni miongoni mwa nchi za kwanza zilizosaini mkataba wa NPT; ilisaini mkataba huo Julai Mosi, 1968. Aidha Februari mwaka 1970 Bunge la Iran baadaye liliuidhinisha mkabata huo na ukaanza kutumika kwa ajili ya Iran baada ya hapo.
Kulingana na mkataba wa NPT, Iran inatambulika kama nchi isiyo na silaha za nyuklia na ilikubali kutotengeneza au kumiliki silaha za nyuklia, ikiwa na haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani chini ya usimamizi wa kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Shughuli za nyuklia za Iran zimekuwa chini ya uangalizi wa mara kwa mara wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).