Oct 15, 2022 11:18 UTC
  • Maelfu ya Wamorocco waandamana kuliunga mkono taifa la Palestina

Maelfu ya wananchi wa Morocco wamefanya maandamano ya kutangaza uungaji mkono wao kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina na msimamo wao imara wa kuihami Baytul Muqaddas na Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Maandamano hayo ya maelfu ya wananchi wa Morocco yamefanyika licha ya kwamba nchi hiyo ilikuwa ya nne ya Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mashinikizo ya Marekani. Nchi nyingine zilikuwa ni Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain na Sudan.

Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, maandamano hayo yameitishwa na kundi la kupigania masuala ya umma na yamefanyika katika zaidi ya miji 20 ya Morocco.

Walioshiriki kwenye maandamano hayo wamelaani ukandamizaji unaoendelea kufanya na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti Mtakatifu wa al Aqsa na wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.

David Govrin, balozi wa Israel aliyekumbwa na kashfa ya ngono nchini Morocco

 

Vile vile wamelaani kimya cha nchi za Kiarabu mbele ya jinai za Israel na kufuata kwao kibubusa siasa za kindumilakuwili za nchi za Magharibi kuhusu kadhia ya Palestina.

Ni vyema kusema hapa kwamba, wananchi wa Morocco hivi karibuni walifanya maandamano mengine makubwa ya kulaani ziara ya waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni mjini Rabat na walichoma moto bendera za utawala huo pandikizi.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita pia, mamia ya wananchi wa Morocco waliandamana mjini Rabat kulaani ufuska wa balozi wa utawala haramu wa Israel, David Govrin, baada ya balozi huyo kukumbwa na kashfa ya ngono.  

Tags