Al-Burhan: Inawezekana kufikia makubaliano kuhusu Bwawa la Renaissance
(last modified Sun, 16 Oct 2022 06:58:43 GMT )
Oct 16, 2022 06:58 UTC
  • Al-Burhan: Inawezekana kufikia makubaliano kuhusu Bwawa la Renaissance

Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ambaye pia ni kamanda wa jeshi la nchi hiyo amesema, kuna uwezekano wa kufikiwa mapatano kuhusu Bwawa na Renaissance.

Jenerali Abdel Fattah al Burhan ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. 

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance kwenye vyanzo vya Mto Nile nchini Ethiopia umezusha mzozo mkubwa wa maji kati ya nchi tatu za Misri, Ethiopia na Sudan.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba sehemu ya maji ya kila moja kati ya nchi hizo itapungua kutoka ujenzi wa Bwawa la Renaissance nchini Ethiopia.

Kwa upande mwingine, Ethiopia inasema ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa nchi na kukidhi mahitaji ya umeme.

Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Al Burhan amesisitiza kuwa, upo uwezekano wa kufikiwa mapatano kuhusu masuala ya kiufundi ya Bwawa la Renaissance.  

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia pia amesema katika mazungumzo hayo kwamba mradi wa Bwawa la Renaissance utakuwa na manufaa mengi hata kwa Sudan yenyewe.

Bwawa la Renaissance

Itakumbukwa kuwa, mazungumzo ya pande tatu kati ya Misri, Ethiopia na Sudan chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika kuhusu mzozo wa Bwawa la Renaissance yameshindwa kufikia mapatano kuhusu kadhia hiyo. 

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance umegharimu dola bilioni tano na ndilo bwawa kubwa zaidi la kuzalisha umeme kwa kutumia maji barani Afrika.

Tags