Ethiopia yazuia matumizi ya fedha za kigeni
Ethiopia imeziagiza benki nchini humo kuwanyima wafanyabiashara fedha za kigeni ambao wanaaagiza bidhaa zisizopewa kipaumbele. Ethiopia imechukua hatua hiyo katika juhudi za kuimarisha akiba yake ya kigeni inayoendelea kupungua siku baada ya siku.
Itakumbukwa kuwa, Ethiopia ni miongoni mwa mataifa yenye uchumi mkubwa barani Afrika. Hatua hiyo inasimamisha uagizaji wa makumi ya bidhaa kama vile pombe na magari huku wafanyabiashara wakilazimika kujisajili katika benki ili kupata pesa za kigeni kwa ajili ya kuingiza bidhaa nchini.
Melaku Alebel Addis Waziri wa Fedha wa Ethiopia ameiandikia barua Benki Kuu ya nchi hiyo akisema: Ni lazima kuzuia matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa zisizokuwa za chakula, dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi na malighafi kwa ajili ya viwanda." Kwa hiyo, tunatuma orodha ya bidhaa ambazo hazitaruhusiwa kwa muda usiojulikana, amesema Waziri wa Fedha wa Ethiopia.
Orodha ya bidhaa zisizopungua 40 zilizotajwa ni pamoja na pikipiki hadi saa za ukutani, miavuli, mazulia, sabuni, pombe, manukato na sigara.
Benki Kuu ya Ethiopia mwezi Machi mwaka huu ilitangaza kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni za nchi hiYo na kufikia dola bilioni 1.6 hadi kufikia mwishoni mwaka jana; kiasi ambacho kingetosheleza tu kuingizwa nchini bidhaa kwa muda wa chini ya miezi miwili pekee.
Mamlaka za Ethiopia hivi karibuni pia ziliimarisha sheria kuhusu umiliki wa fedha za kigeni kwa watu binafsi na biashara na kupiga marufuku shughuli zote za fedha za kigeni nchini Ethiopia.