AU yazitapa pande hasimu Ethiopia kuketi kwenye meza ya mazungumzo
Umoja wa Afrika umetoa wito kwa pande zinazozozana katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani.
Machafuko na vita vilivyoshuhudiwa katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia kati ya jeshi la serikali kuu na wapiganaji wa kundi la waasi la Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) tokeo Novemba 2020 vimepelekea kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ametoa taarifa akisema kuwa kushadidi vita na mapigano huko Tigray kunatia wasiwasi mkubwa.
Moussa Faki Mahamat amezitaka pande husika kufanya mazungumzo ya moja kwa moja nchini Afrika Kusini kupitia timu ya ngazi ya juu inayoongozwa na Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika katika Pembe ya Afrika na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.
Katika matukio ya hivi karibuni, mji wa Shire ulioko kaskazini-magharibi mwa Tigray ulishambuliwa kwa siku kadhaa katika hujuma ya pamoja ya vikosi vya majeshi ya Ethiopia na Eritrea, na idadi kadhaa ya raia wameuawa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres pia ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kushadidi kwa ghasia na athari zake kwa raia huko kaskazini mwa Ethiopia.
Serikali ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na wapiganaji wa Tigray wamekubali mwaliko wa Umoja wa Afrika wa kuketi kwenye meza ya mazungumzo, lakini mazungumzo hayo ambayo yalitakiwa kuanza mwishoni mwa juma lililopita nchini Afrika Kusini, hayakufanyika.
Mazungumzo hayo yalipangwa kufanyika chini ya usimamizi wa mjumbe wa Umoja wa Afrika katika Pembe ya Afrika, Olusegun Obasanjo, akisaidiwa na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Phumzile Mlambo-Ngcuka.