Wasudani wapinga mwenendo wa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel
Katika kikao kinachofanyika mjini Khartoum kuhusu suala la Palestina, makundi ya Kiislamu ya Sudan yametahadharisha kuhusu hatua ya Waarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Washiriki katika mkutano huo wamesisitiza kuwa, suala la Palestina ndilo kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, na kwamba mataifa yote ya Kiislamu yanapaswa kuiunga mkono Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa dhidi ya mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel.
Washiri katika kikao hicho cha Khartoum wameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya jinai katika maeneo mbalimbali ya Palestina ikiwemo Quds Tukufu na kwamba ni muhimu kuwaunga mkono wananchi na mapambano ya Palestina.
Ali Abdullah, kiongozi wa harakati ya Wasudan dhidi ya uhusiano wa Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel amesisitiza kuwa, ardhi ya Palestina ni ya Wapalestina, na utawala wa Kizayuni hauna nafasi katika eneo hilo.
Abdullah ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni umepora ardhi ya Palestina na kubainisha kuwa, suala la Palestina ni suala la mataifa yote ya Kiislamu, na ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kushikamana na kuwa na umoja kuhusiana na kadhia ya Palestina.
Osman Ibrahim, msemaji wa Chama cha Hizbul-Tahrir cha Sudan pia amesema: Ardhi ya Palestina ni ya Wapalestina, na Wazayuni lazima wafukuzwe kutoka katika ardhi hiyo.
Mkutano wa vyama na makundi ya Kiislamu ya Sudan yanayounga mkono ukombozi wa Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa unaendelea mjini Khartoum leo Jumatatu.
Katika siku za hivi karibuni Wazayuni wamezidisha mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwemo Nablus na Msikiti wa Al-Aqsa ambako wanafanya mauaji ya jinai dhidi ya raia wa Kipalestina.