NATO yashambuliwa mitandaoni baada ya kuripotiwa kuua raia laki 5 Libya 2011
Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) limevunja kimya na kutoa taarifa ya kujitenga na ripoti iliyochapishwa na vyombo mbalimbali vya habari na kusambaa katika mitandao ya kijamii kuwa vikosi vya taasisi hiyo viliua malaki ya raia nchini Libya mwaka 2011.
Tovuti ya kuhifadhi kumbukumbu na matukio makubwa barani Afrika ya 'Africa Archives' ilichapisha ujumbe wa Twitter hivi karibuni uliosema kuwa, NATO ilifanya mashambulizi ya anga yapatayo 10,000 mwaka 2011 nchini Libya, na kusababisha vifo vya raia 500,000.
Ujumbe huo ambao umesambaa katika mitandao ya kijamii unaeleza kuwa, NATO ilipoulizwa kuhusu mauaji hayo ya raia wasio na hatia ilisema, hasara za nafsi za aina hiyo ni mambo ya kawaida katika vita.
Hata hivyo NATO bila kutaja idadi ya raia waliouawa katika operesheni zake nchini Libya mwaka 2011, inasema mashambulio hayo hayakuua idadi iliyotajwa ya raia.
Umoja wa Mataifa ulidai huko nyuma kuwa, mashambulizi hayo ya NATO yaliua raia 60 tu, huku shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch likisema idadi ya waliouwa Libya wakati huo ni raia 72, ambapo thuluthi moja walikuwa watoto. Amnesty International nayo ilisema Walibya waliouawa katika hujuma za anga za NATO ni 55, wakiwemo watoto 16 na wanawake 14 katika miji ya Tripoli, Zlitan, Majer, Sirte na Brega.
Libya imekuwa ikikabiliwa na misukosuko ya kisiasa na machafuko tangu jeshi la nchi za Magharibi NATO lilipoivamia nchi hiyo na kuuangusha utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Nchi za Magharibi zilifanya mashambulio ya kikatili dhidi ya Libya, yaliyosambaratisha kabisa miundombinu ya nchi hiyo ya Waislamu na baadaye kuitelekeza huku zikiacha silaha za kila namna zikiwa zimeenea mikononi mwa watu wa mirengo hasimu.
Kila leo tangu wakati huo, mamlaka za Libya zimekuwa zikitangaza habari ya kugunduliwa miili katika makaburi ya umati, zikiwemo maiti15 za watu wasiojulikana zilizogunduliwa mwezi uliopita katika makaburi mawili ya umati kwenye mji wa Sirte, ulioko umbali wa takriban kilomita 450 mashariki mwa mji mkuu Tripoli.