UN yataka kuzidishwa haraka misaada ya kibinadamu huko Somalia
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetoa wito wa kuzidishwa misaada ya kibinadamu ya haraka kwa ajili ya Somalia.
OCHA imetangaza kuwa, ukame mkubwa ulioiathiri Somalia umepelekea kuwepo udharura wa kutolewa misaada ya haraka kwa nchi hiyo. Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayohuisika na uratibu wa masuala ya kibinadamu imeongeza kuwa, hadi sasa kumetolewa dola bilioni moja tu kwa ajili ya kuwadhaminia mahitaji muhimu raia wa Somalia zaidi ya milioni 7 na kwamba hadi mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka kesho wa 2023, kiasi kingine cha dola bilioni moja kitahitajika haraka ili kuweza kutoa misaada mbalimbali kwa wananchi wa Somalia walioathiriwa na ukame mkubwa.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, raia wa Somalia milioni 7 na laki nane ambao ni nusu ya jamii ya nchi hiyo, wamekumbwa na ukame mkubwa huku watu 213, 000 miongoni mwao wakikabiliwa na hatari ya njaa kali.
Huu ni ukame wa tatu kuikumba Somalia katika kipindi cha muongo mmoja wa karibuni; hata hivyo ukame unaoitatiza nchi hiyo kwa sasa unatajwa kuwa mkali na wa kutisha zaidi ukilinganishwa na ukame ulioiathiri nchi hiyo mwaka 2010 hadi 2011 na ule wa 2016 hadi 2017.