Wasudani waendeleza mandamano kupinga utawala wa kijeshi
Maandamano makubwa dhidi ya serikali ya kijeshi nchini Sudan kwa mara nyingine tena yamesababisha mapigano makali kati ya askari usalama na waandamanaji.
Televisheni ya Al Jazeera imeripoti kuwa, idadi kadhaa ya waandamanaji mjini Khartoum, mji mkuu wa Sudan, walijeruhiwa kwa kurushiwa guruneti za moshi na gesi ya kutoa machozi na askari usalama wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yamefanyika Khartoum kutaka kuundwa serikali ya kiraia na kuwawajibisha wahusika wa mauaji ya watu kadhaa walioshiriki katika maandamano kama hayo mwaka mmoja uliopita.
Maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini Sudan yamekuwa yakifanyika karibu kila siku katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo tangu Oktoba 2021.
Sudan ilitumbukia kwenye lindi la machafuko na mapigano kati ya jeshi na raia wanaopinga utawala wa kijeshi, tangu wanajeshi walipofanya mapinduzi Oktoba 25, 2021. Licha ya wanajeshi kuahidi kwamba watakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, lakini wananchi wanaopinga nchi hiyo kutawaliwa na jeshi wanataka majenerali wa jeshi wang'atuke madarakani na nchi hiyo kuongozwa katika kipindi cha mpito na utawala wa kiraia kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia.
Mwezi Septemba mwaka huu pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, wanajeshi wanaotawala nchini Sudan wanapaswa kukabidhi hatamu za uongozi kwa utawala wa kiraia.
Antonio Guterres alitoa msisitizo huo katika mazungumzo yake na Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Mkuu wa baraza tawala la Sudan walipokutana pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.