Wananchi wenye hasira wa DRC wachoma moto magari ya UN
(last modified Wed, 02 Nov 2022 13:10:57 GMT )
Nov 02, 2022 13:10 UTC
  • Wananchi wenye hasira wa DRC wachoma moto magari ya UN

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokuwa na ghadhabu wamechoma moto magari ya askari walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kwa jina la MONUSCO, wakisisitiza kuwa kikosi hicho cha UN kimeshindwa kukabiliana na harakati na mashambulizi ya kundi la waasi la M23.

Wakazi wa mji wa Goma mashariki mwa DRC jana jioni walifanya maandamano na kuteketeza kwa moto magari hayo ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, wakisisitiza kuwa ujumbe wa MONUSCO unapaswa kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, kwani uwepo wake haujasaidia chochote katika kurejesha usalama na uthabiti nchini humo.

Mmoja wa waandamanaji hao kwa jina Kasereka Munyafura amesema, "Kwa sababu ya waasi hawa (wa M23) tumelazimika kuyahama makazi yetu Rugari, Kibumba. Ni kwa msingi huo ndio tuna hasira hivi, tumeyachoma moto magari ya MUNUSCO kwa sababu yanatusababishia matatizo."

Mapema jana Jumanne,  kikosi cha MUNUSCO kilitangaza kuchukua hatua eti ya kistratajia ya kuondoa askari wake mjini Rumangabo. Waasi wa M23 kwa katika wiki za hivi karibuni wamekuwa wakifanya jitihada za kuudhibiti mji huo wenye kambi ya jeshi.

Kwa muda sasa, wananchi wa DRC wamekuwa wakitaka kuondoka askari hao wa kulinda amani, kutokana na kile wanachodai kuwa, ni uzembe katika utendaji wao wa kazi kwa zaidi ya miongo miwili tangu watumwe nchini humo.

Waasi wa kundi la M23

Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, maelfu ya watu wameandamana kwa siku kadhaa sasa katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dhidi ya Rwanda inayodaiwa kuwaunga mkono waasi wa M23, huku uhusiano baina ya nchi hizo mbili ukizidi kuharibika baada ya Kinshasa kumuita nyumbani kaimu balozi wake wa Kigali.

Watu 50,000 wamekimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na karibu 12,000 ambao wamekimbilia usalama wao katika nchi jirani ya Uganda, baada ya kupamba moto mapigano mashariki mwa DRC. DR Congo imeendelea kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda inayakanusha.

 

Tags